top of page
Yachunguzeeni.png
Somo-1-Cover-Pic-278x300.png

03. Wokovu

Siku moja wakati wafanyakazi walipokuwa wanapaka rangi juu ya mnara wa taa, ilitokea ajali ambayo haitasahaulika kwa wale walioiona. Wakiwa juu kiasi cha mita 20, mmoja wao alirudi nyuma kupita kiasi na kuyumba kabla wenzie hawajaweza kumdaka, aliporomoka kwenda chini akiwa na uhakika wa kufa kwenye mawe yaliyokuwepo pale.

Wenzie walishuka upesi. Walipigwa na butwaa walipomkuta yule mtu akiwa ameduwaa lakini amelala chini bila kudhurika. Muujiza huu ulisababishwa na kondoo waliokuwa wakila chini ya ule mnara. Mwili laini wenye sufu wa kondoo mkubwa, ulituliza anguko na mtu yule aliyekuwa katika hatari ya kufa, badala ya kufa mtu yule alikuwa ameduwaa; lakini kondoo alikuwa amekufa.

Mfanyakazi aliyeanguka ni mimi na wewe. Kondoo aliyekufa anawakilisha kile ambacho Yesu, Mwana-Kondoo wa Mungu, alikifanya kutuokoa kutoka kifo cha hakika. Wanadamu wote walikabiliwa na kifo cha hakika baada ya Adamu na Hawa kuasi na kutengwa na mti wa uzima. Mwanzo 3:22-24 inatueleza kuwa Mungu alimtenga mwanadamu na chanzo cha uzima baada ya kutenda dhambi ili asiishi milele: “BWANA Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wfa uzima, akala, akaishi milele; kwa hiyo BWANA Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.” Mwa. 3:24. Hii ndiyo adhabu ambayo Adamu alikuwa ameambiwa kabla ya kuasi.

Lakini Mungu aliwapatia habari njema alipomwambia nyoka, “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke; na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino” (Mwa. 3:15).

Mungu alitabiri kuwa pambano lililokuwa limeanza mbinguni, lingeendelea. Nyoka angeujeruhi uzao wa mwanamke, yaani, Kristo. Jeraha lingeuma, lakini lisingeua. Kwa wakati wake, Kristo naye angeponda kichwa cha nyoka na kumrejesha mwanadamu katika familia ya Mungu. Mwana-Kondoo wa Mungu alipaswa kutolewa kafara ili kupata haki ya kumharibu Ibilisi na kazi zake. Tangu mwanzo wa ulimwengu, mpango wa wokovu ulikuwa tayari ili kumhakikishia kila mmoja wetu nafasi ya kuepuka kupotea milele, ambayo ndiyo adhabu kwa ajili ya dhambi. Sasa angalia Biblia inavyoelezea jinsi mpango huu unavyoweza kufanya kazi katika maisha yako.

1. Je, Kristo, Mwana wa Mungu, amekuwepo kwa muda gani?

“Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele” Mika 5:2. “Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” Yn 17:5. “Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.” Zab. 90:1,2.

2. Biblia inasema Yesu, yaani, Neno ni nani?

“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu… Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yn 1:1,14.

3. Lakini, je, Mungu ananijali kweli?

Mungu anasema hivi: “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda.” Isa. 43:4. “Naam nimekupenda kwa upendo wa milele.” Yer. 31:3.

 

4. Je, Mungu ameuonyeshaje upendo wake kwetu?

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” Yn 3:16. “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.” 1 Yoh. 4:9,10.

Kwa kuwa anatupenda sana, yuko tayari kuona Mwanawe akiteseka na kufa kuliko kutenganishwa na wewe na mimi milele zote. Hatutaweza kuelewa, lakini alifanya hivyo kwa ajili yangu na wewe.

5. Angewezaje kunipenda mtu kama mimi?

“Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” Rum. 5:8.

Hakika siyo kwa sababu nimestahili. Hakuna mmoja kati yetu anayestahili cho chote, isipokuwa mshahara wa dhambi ambao ni mauti. “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rum. 6:23).

6. Je, kifo chake kinanisaidia nini?

“Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu.” 1Yoh. 3:1. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake.” Yn 1:12.

Kristo alikufa ili kulipa gharama ya adhabu ya kifo dhidi yangu. Alizaliwa kama mwanadamu ili afe kifo ambacho mimi nastahili. Kisha yale yote anayostahili yeye amenipa mimi.

Kifo cha Yesu kilikuwa ni malipo kamili kwa ajili ya kila dhambi ambayo ungeweza kuifanya. Unapoikubali na kuipokea zawadi hii ya ajabu, unakuwa sehemu ya familia ya Yesu mwenyewe.

7. Ninawezaje kumpokea na kutoka katika mauti kuingia uzimani?

Kiri mambo matatu:

A. Mimi ni mwenye dhambi. “Wote wametenda dhambi” (Rum. 3:23).

B. Niko hatarini kufa. “Mshahara wa dhambi ni mauti” (Rum. 6:23).

C. Siwezi kujiokoa. “Pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote” (Yn. 15:5).

Baada ya toba hiyo amini mambo matatu:

A. Alikufa kwa ajili yangu. “Aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.” Ebr. 2:9.

B. Amenisamehe. “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafsha na udhalimu wote.” 1 Yoh. 1:9.

C. Ameniokoa. “Yeye aaminiye yuna uzima wa milele.” Yn 7:47.

Kwa kuomba, kuamini, na kuipokea zawadi ya Mungu, yaani, Bwana wetu Yesu kristo.

Yatafakari mambo haya kwa muda:

  • Kwa sababu ya dhambi zangu nimehukumiwa kifo.

  • Siwezi kulipa fdia hiyo bila kupoteza uzima wa milele, kwani kama nikifa kwa ajili ya dhambi zangu, sitaweza kujifufua. Nitakuwa nimekufa milele.

  • Ninadaiwa deni nisiloweza kulilipa. Lakini kuna rafki aliyekuja katika nafsi ya Yesu na kusema, “Nitalipa. Nitakufa badala yako na kukuhesabia kuwa umelipa wewe. Huna haja ya kufa kwa ajili ya dhambi zako.”

  • Ni lazima niipokee zawadi hii. Ni rahisi tu. Ninakiri wazi na kukikubali kifo chake kwa ajili ya dhambi zangu. Mara baada ya kufanya hivyo, ninakuwa mtoto wa Mungu.

8. Yanipasa kufanya nini ili niipate zawadi ya wokovu?

“Wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.” Rum. 3:24. “Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.” Rum. 3:28.

Jambo la pekee ninaloweza kufanya ni kuipokea tu kama zawadi. Matendo yangu ya utii hayatanisaidia hata kidogo katika kuhesabiwa haki. Wote watakaoomba wokovu kwa imani wataupata. “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” Efe. 2:8,9.

9. Ninapojiunga na familia yake kwa njia ya imani, Yesu atafanya mabadiliko gani katika maisha yangu?

“Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! yamekuwa mapya.” 2 Kor. 5:17.

Yesu anapopokelewa katika moyo wangu, huiharibu nafsi ya kale ya dhambi na kunibadilisha hasa kuwa kiumbe kipya. Maisha ya kale ya dhambi yanakuwa hayatamaniki tena. Kwa furaha naanza kujisikia huru kutoka katika hatia na hukumu.

10. Hivi haya maisha mapya yatakuwa ya furaha kweli kuliko anasa za maisha ya kale?

Yesu alisema: “Hayo nimewaambia, ili furaha yenu itimizwe.” Yn 15:11. “Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.” Yn 8:36. “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Yn 10:10.

Wengi wanadhani kuwa maisha ya Kikristo si ya furaha, na yana masharti magumu. Ni kinyume cha hayo. Unapompokea Yesu, amani na furaha vitatawala maisha yako.

11. Lakini ninaweza nikafaulu kuyatenda yote ambayo Mkristo anapaswa kuyatenda?

“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu.” Gal. 2:20.

“Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.” Flp. 4:13.

Hapa ndipo ulipo muujiza mkubwa kabisa wa maisha ya Kikristo. Huna haja ya kujilazimisha. Kinachotokea kwako, ni kudhihirika kwa maisha ya mtu mwingine aliye ndani yako. Nia ya Kristo itakuwa ndani yako. Utii hutokana na upendo.

12. Je, una maana hata Amri 10 haitakuwa vigumu kuzishika?

“Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Yn 14:15.

“Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.” 1 Yoh. 5:3.

“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake… Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani yake.” 1 Yoh. 2:3,5.

Biblia mara zote inauoanisha utii na upendo. Wakristo waliozaliwa upya hawaoni taabu kushika Amri za Mungu kwani si wao bali ni Kristo ndani yao. Ukweli ni kwamba, kwa kuwa nampenda sana kwa kubadili maisha yangu, nitafanya zaidi ya matakwa ya Amri 10. Nitaichunguza Biblia ili nijue mapenzi yake nikijaribu kupata njia zaidi za kuonyesha upendo wangu kwake. “Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.” 1 Yoh. 3:22.

13. Nitahakikishaje kuwa kushika amri kunakotajwa katika Biblia kwa ajili ya watu wa Mungu si kufanya matendo ya sheria?

“Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” Ufu. 14:12. “Nao [watakatifu] wakamshinda kwa damu ya MwanaKondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” Ufu. 12:11.

Usichanganye utii na matendo ya sheria. Matendo ya sheria ni kujaribu kupata wokovu kwa kutenda mema. Watakatifu wanaelezewa katika Biblia kuwa wana sifa 4: (1) Kushika Amri; (2) Kuamini damu ya MwanaKondoo; (3) Kushuhudia imani yao kwa wengine; na (4) Kuchagua kifo kuliko kufanya dhambi. Hizi ni sifa za kweli za mtu ampendaye Kristo na kujitoa maisha yake kumfuata.

14. Ni tendo gani muhimu linaloashiria kwamba muumini ameanza uhusiano mpya wa upendo na Kristo, nalo huwakilisha nini?

“Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.” “Ili mwili wa dhambi ubatilike.” Rum. 6:4,6. “Kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimleee Kristo bikira saf.” 2 Kor. 11:2.

Ubatizo huonyesha matukio matatu ya muhimu katika maisha ya muumini wa kweli:

(1) Kuifa dhambi;

(2) Kuzaliwa upya katika Kristo; na

(3) Kuolewa na Kristo milele. Muungano huo wa kiroho utazidi kukomaa na kuwa mtamu zaidi kadiri muda unavyokwenda, na kadiri upendo utakavyozidi kukua.

15. Nitahakikishaje kuwa imani na upendo wa ndoa yangu na Kristo utadumu na kuongezeka?

Yachunguze Maandiko. “Mwayachunguza Maandiko.” Yn 5:39. “Ombeni bila kukoma.” 1 The. 5:17. “Kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye.” Kol. 2:6. “Ninakufa kila siku.” 1 Kor. 15:31.

Hakuna mapenzi yanayoweza kudumu bila mawasiliano. Maombi na kusoma Biblia ni mambo ya lazima ili uhusiano huu uendelee kudumu. Neno lake ni barua ya upendo ambayo ninapaswa kuisoma kila siku kudumisha maisha ya kiroho.

Mungu hutia muhuri ndoa yetu ya kiroho. Ili kutia muhuri ndoa yetu ya kiroho, ameahidi: kuwa hataniacha (Zab. 55:22Mt. 28:20Ebr. 13:5), kuwa atanitunza katika ugonjwa na katika uzima (Zab. 41:3Isa. 41:10), na kuniptia mahitaji yote yanayoweza kutokea katika maisha yangu (Mt. 6:25-34). Kama nilivyompokea kwa imani na kuziona ahadi zake kuwa zinatosheleza, naendelea kumwamini kwa kila hitaji lililo mbele yangu na hajawahi kuniangusha.

Mungu amewapa wanadamu thamani kubwa ajabu! Kwa njia ya uasi, wana wa Adamu waliwekwa chini ya Shetani. Lakini kwa njia ya kafara ya upatanisho ya Yesu Kristo, wana wa Adamu wanaweza kuwa wana wa Mungu. Upendo kama huu hauna kifani. Kuwa watoto wa Mfalme wa Mbinguni! Ahadi ya thamani! Suala la kutafakari kwa kina sana! Upendo wa Mungu usio kifani kwa ulimwengu ambao haukumpenda!

Baada ya kujifunza juu ya maisha na kafara ya Kristo, je, ungependa kumkaribisha aingie katika maisha yako, na kuzaliwa upya?

1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15

bottom of page